TMAA yapongezwa kusimamia madini

WATENDAJI kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha India (NDC) wamepongeza Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa umakini wake katika usimamizi na ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini.

Kiongozi wa ujumbe huo, Admiral Sudan alitoa pongezi hizo katika kikao kilichofanyika makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam wakati ujumbe huo ulipokutana na watendaji wa TMAA wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.

Ujumbe huo kutoka India, ulifika wizarani kujifunza namna TMAA inavyosimamia shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini. Walielezwa namna inavyofanya kazi nzuri, ikiwa mwangalizi wa madini nchini hasa katika juhudi zake za udhibiti wa utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi.

Awali, Meneja wa Mipango na Utafiti wa TMAA, Julius Moshi, aliwaambia Julai 2015 hadi Machi 2016, jumla ya kilo 1,114.49 za dhahabu zenye thamani ya Sh bilioni 73.5 zilizalishwa na mrabaha wa Sh bilioni 2.9 kulipwa serikalini kutokana na shughuli hizo za uchenjuaji madini.