Watakaowapa leseni majirani bila utaratibu kukiona

WATUMISHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, mkoani Katavi, watakaobainika kutoa leseni za uvuvi kwa raia wa nchi jirani bila kufuata utaratibu watachukuliwa hatua kali. Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM).

Mbunge huyo alitaka kujua kwa nini raia wa nchi jirani wanapewa leseni za uvuvi kwa ada ambazo ziko sawa na zile wanazolipa wananchi wa Tanzania. Akijibu swali hilo, Nchemba alisema, tayari amepata taarifa kuwa wavuvi kutoka nchi jirani wanavua Tanzania na utaratibu wa kuwatambua unafanyika.

Nchemba alisema watumishi wa halmashauri watakaobainika serikali itachukua hatua. Pia akiuliza swali la nyongeza Mbunge wa Kigamboni Dk Faustine Ndugulile (CCM) alihoji serikali ina mpango gani wa kuondoa kodi kwa wavuvi kwani zimekuwa nyingi.

Akijibu swali hilo, Nchemba alisema wizara inaangalia maeneo yote yanayolalamikiwa kutokana na kuwa na leseni nyingi. Alisema pia suala la leseni kutolewa kwa dola litaangaliwa kwani nalo halikubaliki. “Tutafanyia kazi changamoto zote na tutatoa tamko,” alisema Nchemba.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Malindi, Ally Sahe (CUF) alihoji kwa nini wavuvi wa Unguja wameanza kusumbuliwa na kuwekewa vikwazo vya kuvua maeneo ya Tanzania Bara.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, William ole Nashe, alisema shughuli za uvuvi kwenye maji ya kitaifa na maji baridi si moja ya suala la Muungano hivyo uvuvi katika maji hayo husimamiwa kupitia Sheria za Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 kwa upande wa Tanzania Bara na Sheria ya Uvuvi namba 7 ya 2010 kwa upande wa Zanzibar.